FDT yawasilisha Tafiti za Fulsa kwa Wawekezaji wa mazao ya Miti

FDT yawasilisha tafiti fursa za uwekezaji

  • Mtanzania
  • 1 Oct 2019
  • Na FRANCIS GODWIN

TAASISI ya Uendelezaji Misitu Tanzania (FDT), imewasilisha utafiti waliofanya wa kuangalia fursa za uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji wa ‘plywood’ na mazao ya misitu kwa wawekezaji kutoka nje ya Tanzania na wazalendo waliowekeza Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.

Akizungumza baada ya mtafiti kutoka nchini Australia, Mihai Dhaihan kuwasilisha utafiti wa fursa katika uwekezaji wa viwanda vya kutengeneza plywood kwa matumizi ya ujenzi na samani mbalimbali jana, Meneja wa Uendeshaji Masoko FDT Mkoa wa Iringa, William Mato, alisema lengo la kufanya tafiti hizo ni kutaka kuvuta zaidi Watanzania kuwekeza sekta ya viwanda vya kutengeneza bidhaa hizo.

Alisema katika uwasilishaji wa tafiti hizo zilizofanywa na taasisi yake, wawekezaji 10 wenye viwanda kutoka nje na ndani ya nchi na wale ambao wana mwelekeo wa uwekezaji wa viwanda hivyo wameshiriki.

“Lengo la kufanya tafiti hizi ni kutaka kujua taarifa za undani za uwekezaji wa viwanda, hali ya soko la bidhaa ulimwenguni.

“Tanzania imekuwa na misitu mikubwa hasa ya kupandwa, kumekuwa na viwanda vya kuchakata mbao na bidhaa nyingine, sekta ya misitu imekuwa na mwamko mdogo,” alisema Mato.

Alisema taasisi hiyo iliamua kufanya utafiti ili kuangalia jinsi ya kuwekeza zaidi katika uchakataji wa bidhaa mbadala za mazao ya misitu. Mato alisema walilazimika kufanya utafiti wa miezi mitatu kwa kuangalia fursa zilizopo katika uwekezaji huo na changamoto zake.

Alisema Tanzania kuna viwanda vya kuchakata bidhaa ya plywood zaidi ya 12, vingi vipo Wilaya ya Mufindi, lakini ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji huo ni mdogo.

Mato alisema wawekezaji wengi wanatoka China kutokana na ufahamu wao wa fursa zilizopo, teknolojia na utaalamu wa uendeshaji.

Alisema kuanzishwa kwa viwanda hivyo kwa wingi vinatoa fursa kwa mkulima kuuza sehemu kubwa ya mti kwani hakuna mabaki ambayo hayatatumika kama ilivyo kuwa awali na pia itamwezesha mkulima kuuza miti muda mfupi zaidi wa miaka sita tofauti ya awali ambapo walikuwa wakisubiri kuvuna miti kwa miaka 10.

Marejeo: https://www.pressreader.com/tanzania/mtanzania/20191001/281694026515694