Kipi Bora Kununua Ardhi Tupu Au Shamba lenye Miti Kwenye Mitibiashara?

Kilimo cha Miti kama ilivyo kwa mazao mengine kinahitaji maandalizi ya kina kabla ya kuanzisha shamba. Shamba lililoandaliwa vizuri huleta tija kwenye mazao lakini pia hurahishisha shughuli za upandaji na kuhudumia Miti shambani. Miti pandwa kama Mipaina/Misindano (Pines) na Mikaratusi/Milingoti (Eucalyptus) inayopandwa zaidi kwenye maeneo ya Nyanda za Juu kusini ni moja ya mazao yanayochukua muda mrefu.


Hivyo kilimo cha Miti sio cha kujaribu kwani makosa madogo yanaweza kuleta hasara kubwa kwa mwekezaji. Muhimu zaidi kuzingatia yafuatayo;

 • Kupata taarifa na elimu sahihi ya kilimo cha Mitibiashara.
 • Kupata ardhi yenye rutuba na hali ya hewa inayowezesha miti kustawi vyema.
 • Kuzingatia matumizi ya mbegu na miche bora katika upandaji sahihi wa Mitibiashara.
 • Usimamizi sahihi wa shamba la Mitibiashara na namna ya kuliteka soko la mazao ya misitu.

Shauku ya wawekezaji wengi kwenye Mitibiashara ni kupata shamba bora na lenye muelekeo wa kupata mazao bora. Hivyo wengi wetu huwa na hofu iliyochanganyika na matumaini ya kupata faida nzuri kutokana na uwekezaji kwenye Mitibiashara. Mambo haya hupelekea kufikiri ni kipi bora kati ya kununua shamba lenye miti au ardhi tupu ili upande miti?

Naomba leo niwape machache kuhusiana na swali hili na kusaidia angalau kutoa mwanga utakaoweza kukusaidia katika maamuzi yako. Ningependa kunukuu msemo huu usemao ‘Kupanga ni Kuchagua’. Rejea ya msemo huu inayotoa tafsili isiyo rasmi ni kwamba katika Maisha ya mwanadamu kuna mambo mengi ambayo kila mmoja wetu anaweza kuyafanya, lakini ili aweze kuyafanya vyema ni lazima achague machache na kuzingatia mfumo/mpangilio wa Maisha yake. Kama muelimishaji naweza sema hakuna maamuzi ambayo sio sahihi kama yatakuwa yamechaguliwa vyema.

Mitibiashara kama ilivyo kwenye biashara nyingine ni lazima shamba lako liwe na mpangilio unaofaa kulingana na SOKO husika. SOKO ni kitu cha kwanza kuzingatiwa kwani ndio kitu pekee kinachotoa mwanga wa aina ya mazao, ubora na muda muafaka wa kufanya biashara. Nataka kuorodhesha baadhi ya faida na changamoto mwekezaji anaweza kuzipata kutokana na machaguo haya mawili.

KUNUNUA ARDHI NA KUPANDA MITI.

Hapa namaanisha mwekezaji anafaya maamuzi ya kununua ardhi ili aweze kupanda miti kwa ajili ya kilimo cha Mitibiashara.

Faida;

 • Ghalama ndogo katika uwekezaji wa mwanzo na inampa mwekejaji kuchagua ardhi yenye ubora. Hapa ghalama zaidi itakuwa kwenye ununuzi na usimamizi wa upandaji wa miti kwenye shamba.
 • Kufahamu na kuijua vyema historia ya shamba lake. Hili ni muhimu kwenye taarifa za umiliki na pia kufamu changamoto zilizojitokeza hapo kabla ya kupanda miti.
 • Anaweza kuamua ni aina ya miti na upangaji wa shamba lake la mitibiashara. Maamuzi ya aina gani ya miti itakayopandwa mara nyingi hutegemea mahitaji ya SOKO.
 • Kuwa na uhakika na matumizi ya mbegu bora kwenye shamba. Ili kupata mazao yenye ubora na tija ni muhimu kuzingatia matumizi ya mbegu bora zilizo na sifa kumudu magonjwa, kunyooka, matawi machache na zenye kukua kwa haraka.
 • Kupanda miti katika vipindi tofauti, vyenye malengo na mpangilio mzuri utakaosaidia wakati wa uvunaji. Ukiwa na mapangilio mzuri wa upandaji wa miti, hili litakuwezesha kujipanga vizuri wakati wa uvunaji na uuzaji wa mazao yako. Kwani uwekezaji mzuri ni ule wenye uwezo wa kuliteka SOKO na hili linawezekana kwa kuzalisha mazao ya aina tofauti yenye umli tofauti pia.

Changamoto;

 • Huchukua muda zaidi wa kusubili hadi kuvuna. Mwekezaji ataanzia kwenye shughuli za ununuzi wa ardhi, maandalizi ya upandaji hadi utunzaji wa shamba ambao unahitaji muda na usimamizi wa karibu zaidi.
 • Unahitaji ufuatiliaji wa karibu hasa hatua ya upandaji miti shambani. Shughuli za manunuzi ya ardhi na upandaji wa miti huitaji muda zaidi kutoka kwa mwekezaji kwani ndio jambo la muhimu la kuzingatiwa ili kuleta mazao bora.

KUNUNUA SHAMBA LENYE MITI.

Mwekezaji ananunua shamba ambalo tayari limepandwa miti. Miti hii inaweza kuwa ya kuanzia umli wa miezi au miaka kadhaa. Mara nyingi bei ya shamba huongezeka kutokana na umli wake.

Faida;

 • Huchukua muda mfupi kwenye uwekezaji. Kama mwekezaji atanunua shamba lenye miti likiwa na umli wa miaka Mitano basi atakuwa na muda mfupi wa kusubili mavuno.
 • Hupunguza muda wa ufuatiliaji kwa mwekezaji. Anaweza kutembelea shamba mara TATU au MBILI kwa mwaka, hasa katika shughuli za usimamizi wa shamba na utengenezaji wa njia za MOTO.

Changamoto;

 • Ghalama kubwa katika uwekezaji wa mwanzo. Ghalama ya shamba lililopandwa miti ni kubwa ulikingalisha na kununua ardhi bila miti.
 • Sio rahisi kufahamu historia ya shamba kwa undani. Hili linaweza kukupa ugumu katika kukabiliana vyema na baadhi ya changamoto hasa za umuliki na ukuaji wa miti.
 • Mwekezaji hataweza kuwa na wasaa mzuri wa kuchagua aina ya miti na pia kuwa na uhakika kama miti hiyo ilioteshwa kwa kutumia mbegu bora.
 • Kuwa na uwezekano mdogo wa kupata shamba lenye aina zaidi ya moja na umli tofauti wa miti. Hili litampa mwekezaji uwezo mdogo wa kulimudu SOKO kikamirifu wakati wa mavuno.

Baada ya kusoma na kufahamu faida na changamoto za kila wazo nafikiri ni wakati muafaka kwako kuchagua njia ambayo ni sahihi katika mpangilio wako wa uwekezaji. Kumbuka muda muafaka kwa ajili ya upandaji wa Mitibiashara kwa maeneo ya nyanda za juu kusini ni kuanzia mwezi Disemba hadi Machi, kipindi ambacho miti inapata mvua za kutosha.