Matukio ya moto katika mashamba ya miti na njia za kuthibiti yasitokee

Kila aina ya uwekezaji una changamoto zake. Kwenye kilimo cha miti kuna changamoto kadha wa kadha lakini leo kwa uzoefu wangu nitaongelea changamoto ya moto.
Katika kilimo cha miti, moto ndiye adui mkubwa nambari moja. Moto unaweza kuteketeza maelfu ya ekari za miti ndani ya muda mfupi sana.

Vyanzo vya moto?
Moto unaweza kuanzishwa na mtu mmoja au kikundi cha watu kwa kukusudi ya kulipiza kisasa kutokana na dhuluma au kwa bahati mbaya moto unaweza kumshinda mtu aliyeuanzisha kwa nia ya kusafisha shamba, mfano kwa wakulima wengi wa Nyanda za juu kusini hulima kwenye mabonde wakati wa kiangazi maarufu kama vinyungu.

Wakati mwingine moto husababishwa na migogoro ya ardhi hasa pale ambapo hakuna uwazi na ushirikishwaji wa wanafamilia wote na hivyo wanafamilia ambao hawakushirikishwa huamua kuchoma miti iliyopandwa katika shamba hilo ili kumkatisha tamaa aliyenunua shamba ili aondoke.

Moto unaweza kusababishwa na warina asali wanaotumia moto kufukuza nyuki au wawindaji wenye lengo la kutumia moto kuwafukuza wanyama pori kuelekea sehemu waliyoweka mitego yao na baada ya kazi hiyo huacha moto ukiendelea kuwaka au wanaweza kuuzima lakini yakawepo mabaki ya majivu yenye moto ambayo huweza kukolezwa na upepo na kisha husababisha moto mkubwa ambao huleta uharibifu katika mali za watu.

Tunawezaje kuzuia matukio ya moto?
Zipo njia mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa kuthibiti suala la moto kama ifuatavyo:

  1. Kufuata sheria ndogo za vijiji wakati unaponunua shamba la kupanda miti, lengo likiwa ni kupatiwa uhakika wa umiliki wa ardhi kwa mtu anayekuuzia shamba na kujua mipaka ya ardhi unayouziwa.

  2. Weka barabara za kuzuia moto zenye upana utakaozuia moto kuruka kutoka shamba moja kwenda jingine katika kipindi chenye hatari zaidi ya kuwepo kwa moto kuanzia Mwezi Juni hadi Novemba kila mwaka.

  3. Shirikiana na serikali ya kijiji kwa kuwafanya kuwa sehemu ya umiliki wa mashamba yako, mfano unaweza kuingia makubaliano na kijiji kuwa shamba lako lisipoungua moto na miti ikafikia hatua ya kuvunwa utakipatia kijiji asilimia fulani ya mavuno.

  4. Shauriana na serikali ya kijiji chako kuwe na kamati maalum ya moto na kama inawezekana kila aliyepanda miti katika kijiji hicho achangie katika mfuko wa kuthibiti moto ambao utakuwa na fedha za kugharimia shughuli za moto mfano chakula, kuleta maji ya kuzimia moto wakati wa tukio, kukodi usafiri wa kuwapeleka watu eneo la tukio, pia pesa hizo zitasaidia kamati ya moto kufanya ukaguzi wa mashamba ya miti, kuwakumbusha wenye mashamba wakati wa kuweka njia za kuzuia moto na pia kuchukua hatua kwa wale wanaokaidi kufanya hivyo.

  5. Wasaidie wanakijiji wenye mashamba kuzunguka shamba lako wapande pia miti ili kuwe na nguvu ya pamoja katika kupambana na moto kwani vita ya moto haitakuwa ya kwako peke yako bali ya wanakijiji wote. Mfano unaweza kugharamia mafunzo na kuwapatia miche ya kupanda lengo likiwa kufanikiwa pamoja na kupunguza chuki ya kuwa wewe unataka kufanikiwa pekeyako.

5 Likes

asante sana kwa hii mada, moto ni tatizo kubwa sana kwenye kilimo cha miti wakulima wenzangu. Tubuni kwa pamoja mbinu za kuzuia moto hasa kwa kusafisha mashamba na kuweka barabara za moto

1 Like

Nashukuru sana kwa somo zuri.

Kwa unyeti wa tatizo mimi nafikiri serikali ingeweka vikundi au watu maalum kwa ajili ya kuzima moto kwenye mashamba yetu, hili litasaidia sana hasa kwa sisi tuliopo mbali na mashamba.

Pia napendekeza kuweka sheria kali hasa kwenye maeneo yenye mashamba ya miti ili kuwazuia watu kuwasha moto ambao unaweza kusababisha madhala.

2 Likes

Wadau natumaini mko poa kabisa.
Tarehe 04/10/2018 ilikuwa ni siku muhimu kwa wadau wa kilimo cha miti pale FDT walipoandaa kikao kilichowakutanisha wadau wote kama vile Mameneja wa Misitu wa Wilaya za mkoa wa Njombe, Maafisa Misitu wa Wilaya za Mkoa wa Njombe, wataalam kutoka SUA, FDT, Viongozi wa serikali za vijiji, watendaji wa serikali za vijiji, watoa huduma katika sekta ya misitu na watu waliowekeza kwenye kilimo cha miti ili kujadiliana namna janga la moto linavyoweza kukabiliwa.

Serikali za vijiji walitoa njia nzuri sana, kuanzia matumizi ya sheria ndogo ndogo, kuweka motisha kwa wanaowakamata wale wachoma moto wasiokuwa na vibali na pia kuwa na mifuko ya kukabiliana na moto inayochangiwa na wadau ili kufanikisha ununuzi wa vifaa vya kuzimia moto, usafiri na hata chakula pale tukio linapochukua muda mrefu.
Hongereni sana wadau
image

4 Likes

Jambo zuri sana hili kwa sisi wadau wa Miti kwa upande huu wa nyanda za juu kusini, nafikiri tukiungana vyema tunaweza kukabiliana kwa urahisi na majanga ya moto ambayo ni hatari sana kwenye kilimo cha Miti.

Ombi langu ni kwa serikali iweze kutuunga mkono pale tunapoweka mikakati hii vizuri ili Ile na muendelezo.

2 Likes

Kwa upande wangu naona kama hawa wadau wamechelewa hivi, suala la matukio ya moto yametusumbua sana kwenye miaka miwili iliyipita na kupelekea kupoteza fedha nyingi sana kwenye mashamba yetu ya miti hivyo ni matumaini yangu kuwa kwa mipango hii wakulima tutakuwa salma katika suala la moto.

2 Likes

Ni kweli kabisa unachokisema mdau ila tukumbuke kuwa kila anayejihusisha na kilimo cha miti pia anatakiwa aungane na wadau wote katika juhudi za kutatua suala la matukio ya moto. Hivyo tuzisaidie serikali za vijiji kuja na mipango inayotekelezeka ili mwisho wa siku kila mtu afikie malengo yake

2 Likes