Ukifuata Haya Hutaweza Kutapeliwa Kwenye Uwekezaji Wa Mitibiashara

Kwa ujumla kasi ya uwekezaji katika sekta ya misitu inapamba moto katika maeneo mengi hapa nchini. Kwani katika kipindi hiki kumekuwa na kasi kubwa katika ongezeko la viwanda hasa katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini. Ongezeko hili limechochea zaidi soko la mazao ya miti na kuleta tija kwenye kilimo cha mitibiashara. Sekta ya misitu hadi sasa inajumuisha aina nyingi za miti pandwa hasa Mipaina (Pinus patula) kwa zaidi ya asilimia 80 pia Mikaratusi/Milingoti (Eucalyptus glandis) kwa asilimia 15 na aina nyingine kwa kiasi.


Ni ukweli kwamba biashara ya mazao ya miti haijawahi kushuka katika soko la dunia, vile vile kwenye soko letu la ndani ya nchi. Hili limepelekea watu wengi kuchangamkia hii fulsa ya uwekezaji katika MitiBiashara. Na ukweli usiopingika hasa kwa shuhuda kutoka kwa wawekezaji hawa kwamba hawajawahi kuacha kuongeza kuwekeza kwenye sekta hii. Hivyo kutupa uhakika wa faida na usalama zaidi wa aina hii rahisi ya uwekezaji. Baada ya kupanda miti yako shughulii za uangalizi zinahitaji muda kidogo angalau kutembelea shamba angalau mara TATU au MBILI kwa mwaka.

Kama ambavyo tunafahamu wawekezaji wengi wana majukumu mengine na kuwapa muda mchache wa ufuatiliaji na uangalizi wa mashamba yao kwenye Mitibiashara. Mambo yafuatayo yataweza kuondoa kabisa uwezekano wa kutapeliwa wakati wa ununuzi wa ardhi na usimamizi wa shamba lako kwenye Mitibiashara;

a) Angalau ufahamu jeographia ya eneo husika ambalo unafikilia kwenda kununua, hili utaweza kulipata kutoka kwenye ramani ya nchi, mkoa au vijiji. Pia unaweza kutumia google map kupitia computer au hata kwenye simu yako. Hapa utaweza kutambua mambo ya muinuko, miundo mbinu ya barabara na maji, umbali pia hata uoto wake.
b) Usilipe fedha kwenye siku ya Kwanza, hapa namaanisha watu wengi huwa tunakuwa na mihemko hasa siku ya kwanza hivyo ili kupata taarifa zaidi na kujiridhisha basi ni vyema kujipa muda zaidi katika kufanya malipo. Hakikisha umekutana na uongozi wa Kijiji na umepata fomu maalumu kwa ajili ya mauziano kutoka Serikali ya Kijiji husika
c) Mashahidi ni muhimu sana katika mauziano, hivyo hakikisha umezingatia kupata mashahidi wasio na shaka. Zingatia angalau mashahidi wawili toka upande wako (vyema wakatoka nje ya kijiji husika). Pia hakikisha wamiliki wanne unaopakana nao unawafahamu na angalau wawili wanakuwa ni mashahidi upande wa Muuzaji.
d) Hati za Kimila ni muhimu sana katika uwekezaji wa Mitibiashara kwani zitakuwezesha kupata amana na uhakika katika huduma zingine katika ardhi pamoja na mazao yako. Hili linawezekana kwa kufuata taratibu za mauziano kukamilika katika ofisi ya Kijiji na nyaraka kupelekwa halmashauri kwa ukamilishaji wa hati.
e) Hakikisha unashiriki kikamirifu katika shughuli za maendeleo ya Kijiji husika, kwani wewe sasa ni mmoja wa wanakijiji hapo. Hili litakupa nafasi nzuri ya kufahamu zaidi tabia za wananchi wa eneo husika na kukuwezesha kuishi nao vyema. Kwa sasa vijiji vingi pia zimeunda kamati za MOTO ambazo ni muhimu sana kwenye ulinzi wa mashamba ya mitibiashara. Kamati hizi hufanya doria na pia kusimamia shughuli za uzimaji moto pale unapotokea.
f) Wakati wa uwekezaji ni vyema ukawatumia watoa huduma (Service Provider) wanafahamika na kujulikana na Kijiji. Hili litasaidia kupata watu sahihi na kufanya kazi kwa ubora. Kwani sasa uwekezaji kwenye Mitibiashara sio wa kimazoea hivyo hakikisha msimamizi wa shamba lako awe na ufahamu wa kutosha kuhusu sekta ya misitu. Hili litasaidi kukupa muongozo wenye tija katika njia bora za uandaaji wa shamba, aina na kupata mbegu bora pia hata kwenye usimamizi mzuri wa shamba lako.

Kwa ufupi haya ni baadhi ya mambo ya msingi ambayo yakifuatwa na kuzingatiwa kwa uhakika utakuwa umejihakikishia usalama wa uwekezai wako katika Mitibiashara.

Kumbuka pia ofisi ya Kijiji ni msimamizi mkuu wa vyanzo vya mapato na usalama hivyo Mtendaji na Mwenyekiti wa Kijiji au Kitongoji ni mlinzi wa eneo lake.