Umuhimu wa njia za moto kwenye mashamba ya miti

Njia za Moto (Firebreak/lines)

Njia za Moto (Firebreak/lines) - ni nafasi iliyopo kati ya uoto au vitu vinavyoweza kuwaka/kushika moto na inayoweza kuzuia au kupunguza uwezekano wa Moto kushika au kuwaka. Njia za moto hutumika kuyalinda mashamba ya miti hasa ya miti pandwa kama mipaina/pines, milingoti/mikaratusi na aina nyingine ya miti kutokana na moto kichaa/msituni

Mambo makuu mawili ya kuzingatia ni ;

 • Umbali wa njia ya moto angalau iwe na upana wa mita 5 kwa njia ndogo za kutenganisha ploti moja na nyingine zisizozidi ukubwa wa heka 10. Pia njia za moto zinazotenganisha shamba moja na jingine ziwe na njia za moto zenye upana wa mita 10 na zaidi ili kuzuia uhamaji wa moto kirahisi.
 • Muda muafaka wa kutengeneza njia za moto ni wakati wa palizi/kupalilia hii inasaidia kuweza kuondoa nyasi au miti iliyoota kwenye njia za moto kirahisi na pia ni lazima zipaliliwe tena wakati wa kiangazi hasa kuanzia mwezi Juni na Julai ili kuhakikisha zipo safi na salama kwa kuzuia moto.

AINA ZA NJIA ZA MOTO

 1. Njia za moto za asili - Njia za moto zinaweza kuwa za asilia sehemu ambazo hazina uoto au vishikamoto kama vile mito, ziwa au mkondo wa maji.
 2. Njia za moto za kutengenezwa - Pia zinaweza kuwa za kutengenezwa na binadamu na nyingi wa hizi zinaweza kutumika kama barabara za kutenganisha mashamba ya miti, barabara za kuvunia miti au barabara za njia kuu.

AINA YA NJIA ZA UZUIAJI WA MOTO KWENYE SHAMBA LA MITI

 1. Uzuiaji wa Moto nje ya shamba
  Uzuiaji wa moto nje ya shamba ni njia muhimu na yenye tija katika kuyalinda mashamba ya miti kutokana na moto kichaa. Maeneo mengi ya nje ya mashamba la miti yamezungukwa na uoto wa asili kama vile nyasi poli, miti ya asili, hifadhi za maliasili na mazao ya mengine ya kilimo. Njia nzuri na inayofaa kwa zoezi hili hutokana na aina ya mazingira yaliyolizunguka shamba la miti na pia vifaa vinavyotumiwa kwa kazi hii.

Njia zifuatazo zinaweza kutumika kutengeneza njia za moto;

 • Uchomaji moto wa nyasi au uoto unaolizunguka shamba la miti.
 • Kupanda miti iayoweza kuzuia moto kuzunguka shamba la miti.
 • Kulima njia za moto kwa upana usiopungua mita 5/ miguu 5 au futi 16.
 • Kuvuta na kutoa nyasi ndani ya njia za moto.
 • Kukwangua barabara na mipaka ya mashamba.
 1. Uzuiaji wa Moto ndani ya shamba.
  Ni lazima kupunguza madhala ya moto ndani ya shamba la miti kuliko kutegemea njia za moto iwapo moto utaanzia ndani ya shamba. Moto unaweza kuanzia ndani ya shamba la miti na hapa utengenezaji wa njia za moto za ndani unahitajika zaidi.
  Lakini hili linahitaji uangalizi mkubwa na linaruhusiwa kwenye mashamba yenye eneo dogo tu. Unashauriwa kulima njia za moto ndani ya shamba, kusafisha mipaka ya shamba, kuchoma nyasi/uoto pembezoni mwa maeneo yenye unyevu/maji kama mito au mabwawa. Pia unaweza chepusha maji yanayotembea kama yapo ili kuweza kusaidia kuzuia na kuzima moto. Kuondoa na kuhamisha miti au uoto pia kunasaidia kuzuia moto ndani ya shamba la miti.

KWANINI NI MUHIMU KUWEKA NJIA ZA MOTO?

Sababu kubwa ya kuweka njia za moto ni kuzuia uwezekano wa moto kusambaa kwenye mashamba mengine, pia ni kupunguza nguvu ya moto wenyewe. Umuhimu mwingine ni kulinda uoto wa misitu na kupunguza madhala ya uchafuzi wa hali ya hewa duniani. Jingine kubwa na muhimu kwa mkulima au mmiliki wa shamba la miti ni kulinda miti ili kuongeza pato lake kutokana na biashara ya mazao ya Miti.

KIKOSI CHA KUZIMA MOTO

Kikosi cha zima moto ni muhimu kuandaliwa na kupewa mafunzo muhimu ya mwanzo na mbinu muhimu za kuzima moto wa msituni. Kwa kawaida kikosi cha kuzima moto wa msituni kinahitaji kufahamu njia mbalimbali za kukabiliana na moto, vifaa, mavazi maalum ya kuzimia moto, matanki ya dawa/maji ya kuzimia moto, pia mawasiliano na usafiri wa uhakika pia ni muhimu kuwapa mafunzo ya mara kwa mara kulingana na mazingira ya eneo husika.
Usalama wa maisha ya binadamu ni kitu cha kwanza kuzingatiwa katika kikosi cha zima moto wawapo kazini. Inasisitizwa kuwa na mawasiliano na ufahamu mzuri juu ya njia za usalama pamoja na sehemu za uokozi inapotokea dhalula. Kikosi kina weza kutenga au kuandaa kwa kuchoma sehemu ya shamba au nje ya shamba ambapo upatikanaji wa hewa safi na kuwezesha watu wote kupafikia kwa urahisi pindi inapotokea dhalula.

Msisitizo zaidi unatolewa kwa usalama wa mtu binafsi kwenye kukabiliana na moto wa msituni. Uvaaji sahihi wa mavazi ya kujikinga (PPE-personal protective equipment) ni muhimu zaidi kwa kujilinda na madhala ya moto. Kwa makadilio ya chini kila mwana kikosi cha zima moto anatakiwa kuvaa nguo maalumu zisizoathirika na moto kirahisi, kofia za usalama, viatu ya kuzimia moto, gloves, maji ya kunywa, miwani ya kujikinga pamoja na kifaa cha mawasiliano mara nyingi huwa ni simu za upepo au simu za kawaida.Smartforestry-Firebreak

3 Likes

Mi nafikiri kuwa njia za moto ni njia mojawapo tu ya kuzuia moto ila kuna wakati kuna mioto mikubwa ambayo inaweza kuruka kutoka shamba moja kwenda jingine kwa kuchangiwa na vitu kama upepo na joto

2 Likes

@Machokodo asante kwa maarifa mkuu, hapa nina wazo la ziada. Kwenye shamba la miti licha ya kuwa na fire breaks, naona kama moto unaweza kunasambaa kwa urahisi zaidi kupitia kwenye Canopy(Juu ya miti) kwa sababu matawi yanakuwa yameshikana au yako karibu ukilinganisha na kwnye ground level. Upana wa njia ya moto naona kama unatakiwa uwe mkubwa zaidi ili kuzuia hii hali. Na je kitaalamu, upana wa njia ya moto unategemea na aina ya miti kwenye shamba au hili likoje?

1 Like